JENGO LA MAHAKAMA YA KAPENGURIA LAZINDULIWA LEO.


Kuzinduliwa kwa jengo la mahakama ya kapenguria katika kaunti hii ya Pokot magharibi katika shughuli inayotarajiwa kuongozwa leo na jaji mkuu Martha Komme, kutatoa fursa bora ya kushughulikiwa kesi mbali mbali na kuharakisha haki kwa wanaowasilisha kesi mahakamani.
Wakizungumza katika mahojiano na kituo hiki maafisa kutoka idara ya mahakama kaunti hii Emily Chepkopus na Emmanuel Kibet wamesema kuwa wamekuwa wakipata wakati mgumu kushughulikia kesi mbali mbali kutokana na uhaba wa nafasi katika mahakama hiyo hali ambayo imekuwa ikipelekea kucheleweshwa kwa haki.
Wamewahakikishia wakazi wa kaunti hii ya Pokot magharibi kuwa idara ya mahakama iko tayari kushughulikia kesi zote ambazo zinawasilishwa mahakamani na kuhakikisha haki kwa waathiriwa huku wakiwataka wakazi kutohofu kutumia mahakama katika kutafuta haki.
Aidha maafisa hao wamesema kesi nyingi ambazo zinawasilishwa katika mahakama hiyo ni kuhusu mashamba ambapo mara nyingi utata hutokea kuhusu urithi kutokana na hali kuwa nyingi ya ardhi kaunti hii hazina hati miliki.