JAMII ZA POKOT NA KARAMOJA KUHAMASISHWA UMUHIMU WA KUISHI KWA AMANI

Uongozi mpya wa wilaya ya Amudat katika mpakani pa kaunti hii ya Pokot Magharibi na taifa jirani la Uganda umeapa kuendeleza uhamasisho miongoni mwa jamii za eneo hilo ambazo ni Pokot na Karamoja kuhusu umuhimu wa kuishi kwa amani.

Akizungumza baada ya kuapishwa rasmi kuchukua uwenyekiti wa wilaya hiyo, Joseph Nang’ole amesema wanalenga kuendeeleza mazungumzo miongoni mwa jamii hizo ili kuziwezesha kutumia kwa pamoja raslimali ambazo zimekuwa zikisababisha mivutano ya kila mara miongoni mwa jamii hizo.

Aidha amesema kuwa wamewasilisha ombi kwa rais wa Uganda Yoweri Museveni kuendeleza oparesheni ya kutwa silaha ambazo zinamilikiwa na wakazi wa eneo hilo kinyume cha sheria katika juhudi za kudumisha amani.

Wakati uo huo Nag’ole amesema kuwa atahakikisha elimu inapewa kipau mbele katika eneo hilo ili kuinua viwango vya maisha ya wakazi.