JAMII YAHIMIZWA KUJITENGA NA TAMADUNI YA UKEKETAJI POKOT MAGHARIBI.

Wito umetolewa kwa wazazi katika kaunti ya Pokot magharibi kujitenga na tamaduni ya kuwakeketa pamoja na kuwaoza mapema wanao wa kike na badala yake kuwapa nafasi ya kuendeleza elimu ili pia waafikie ndoto zao maishani.

Akizungumza katika kikao kilichowaleta pamoja wadau mbali mbali ikiwemo maafisa kutoka shirika la watoto UNICEF pamoja na Men End FGM kilichoandaliwa kwenye mkahawa wa Belmont, mwanzilishi wa shirika la amani la Kepako, Diana Rotich alisema kwamba tamaduni hizi zinaambatana na matatizo mengi na huenda zikaathiri maisha yao ya baadaye.

“Kuna madhara mengi ambayo yanatokana na ukeketaji kama vile ugonjwa wa fistula ambao husababisha mhusika kupitia hali ngumu hapo baadaye akitaka kujifungua. Hivyo tunapasa kukataa maneno haya ya kitamaduni ambayo yanawahatarisha watoto wetu wa kike.” Alisema Rotich.

Kwa upande wake afisa katika shirika la Men End FGM Fred Wanyonyi Wafula alisema kwamba shirika hilo linaendeleza mafunzo kwa vijana wa kiume kuhusu jinsi ya kukabili utamaduni huu kupitia mitandao ya kijamii ili kuwaweka katika nafasi bora ya kueneza ujumbe huu katika jamii.

“Tumeamua kwamba tuwalete pamoja vijana wa kiume na tuwafunze ili wapate habari ya jinsi ya kueneza ujumbe dhidi ya tamaduni hii potovu kwa jamii zao, hasa kwa kutumia majukwaa ya mitandao ili kufanikisha vita hivi dhidi ya ukeketaji na ndoa za mapema.” Alisema Wafula.

Ni kauli ambayo imesisitizwa na mkurugenzi wa shirika la Pads for Education Emmanuel Kiptong’o Lepus ambaye amesema kwamba hatua ya kuwahusisha vijana kwenye vita hivi italeta ufanisi mkubwa na hivyo kuhakikisha mtoto wa kike amechungwa inavyopasa.

“Kuwahusisha vijana katika vita hivi ni muhimu sana katika kuhakikisha kwamba wasichana wetu wanaendelea na masomo kwa sababu ukeketaji huwa ishara kamili kwamba msichana ametosha kuozwa. Hivyo tukihakikisha ukeketaji unakabiliwa itasaidia kuhakikisha masomo ya watoto wetu wa kike.” Alisema Lepus.