JAMII YA SENGWER YAAPA KUMSIMAMISHA GAVANA 2022.


Jamii ya Sengwer katika kaunti hii ya Pokot magharibi imelalamikia pakubwa kutengwa kwa muda mrefu katika siasa za kaunti hii licha ya kuwepo idadi kubwa ya watu wa jamii hiyo katika maeneo mbali mbali ya kaunti hii.
Wakiongozwa na msemaji wa jamii hiyo Dickson Rotich, jamii hiyo sasa imetaka kuwepo mkataba wa maelewano baina yao na jamii ya pokot ili mgombea wa ugavana katika uchaguzi mkuu ujao atoke katika jamii hiyo huku naibu wake akitoka jamii ya pokot.
Rotich amesema kuwa iwapo hilo halitoafikiwa basi watalazimika kumteua mtu kutoka jamii hiyo kugombea kiti cha ugavana ili kukutana na wagombea wengine debeni akipuuzilia mbali madai kuwa jamii hii ina watu wachache katika kaunti hii.
Wakati uo huo jamii hiyo imemtaka gavana wa kaunti hii John Lonyangapuo kutumia kile ambacho imetaja kuwa fursa ya kutokuwepo naibu gavana kumteua mmoja wao kushikilia wadhifa huo katika kipindi ambacho kimesalia kabla ya uchaguzi mkuu ujao.