JAMII YA POKOT YAENDELEA KUELIMISHWA KUHUSIANA NA ATHARI ZA KUKEKETA NA KUOZA MABINTI MAPEMA


Shirika la World Vision limeendeleza shughuli ya kuihamasisha jamii dhidi ya ukeketaji na kuwaoza mabinti mapema katika kaunti ya Pokot Magharibi.
Akizungumza katika hafla iliyoandaliwa katika eneo la Sook kwenye Eneobunge la Kapenguria, afisa katika shirika hilo Teresa Cheptoo amesema World Vision limeanzisha mbinu ya kuwapa zawadi ya mifugo vikundi vinavyopigania ukeketaji ikiwa ni njia mojawapo ya kuwapa motisha zaidi ya kupambana na jinamizi hilo.
Mbali na kuwatia wakazi hao motisha, Teresa ameongeza kwamba mradi wa kuvipokeza vikundi hivyo mifugo utawapiga jeki kiuchumi.
Ametumia fursa hiyo kuwarai wakazi kutupilia mbali ukeketaji na kuwaoza wanao mapema badala yake wakumbatie elimu ya mtoto wa kike.
Hellen Loshang’ura mmoja wa wakazi waliopokea zawadi ya mbuzi ametoa shukrani zake kwa Shirika la World Vision akisema limekuwa lenye manufaa mengi kwa wanafunzi na wanariadha wa eneo hilo.
Kwa niaba ya vikundi hivyo vinane, Hellen ameahidi kuuendeleza uhamasisho dhidi ya dhuluma zozote zinazohusiana na mtoto msichana.