JAMII YA NAIBU CHIFU ALIYEJINYONGA KISHAUNET YATAKA UCHUNGUZI WA KINA KUHUSIANA NA KISA HICHO.


Jamii ya naibu chifu wa Kishaunet katika kaunti ya Pokot magharibi aliyefariki kwa kujinyonga Benson Sialuk sasa inataka uchunguzi kuendeshwa kubaini kilichosababisha kifo cha naibu chifu huyo.
Wakiongozwa na mamake mwenda zake Catherine Sialuk, walipuuza taarifa kwamba huenda marehemu alijitoa uhai kufuatia mgogoro ulioibuka katika kanisa hilo jumapili iliyopita, wakisema kwamba ni mtu ambaye hakupenda kujihusisha na migogoro na wengine.
Mkewe marehemu Gladys Nakum alisema kwamba mmewe hakuweza kufika kanisani jumapili hiyo baada yake kusikia kuwa kulikuwa na vurugu.
“Tunaomba uchunguzi kufanyika ili kubainisha kilichosababisha kijana yetu kujinyonga. Tunasikia tu ikisemekana kwamba huenda alijinyonga kutokana na vurugu ambazo zilishuhudiwa kanisani lakini hata hiyo jumapili hakufika kanisani baada yake kufahamishwa kuhusu kilichotokea. Benson ni mtu ambaye hapendi vurugu.” Walisema.
Wametoa wito kwa wahisani na viongozi mbali mbali kaunti hiyo kuisaidia jamii ya mwenda zake kwani sasa hatima ya elimu ya watoto wake haijulikani na mkewe hana uwezo wa kuendelea kuyashughulikia mahitaji familia yake.
“Tunaomba wahisani kuisadia jamii ya marehemu maana ni jamii changa sana. Ana watoto watatu ambao wako shule ya upili na sasa tuna wasiwasi huenda masomo yao yakatatizika baada ya baba yao kuaga dunia.” Walisema.