JAMII YA KARAMOJA YATAJWA KUWA MWIBA , KWEN NA KARITA.


Wakazi wa jamii za eneo la Kwen mpakani pa kaunti ya Pokot magharibi na taifa jirani la Uganda wamelalamikia kukithiri utovu wa usalama eneo hilo hasa unaohusu wizi wa mifugo.
Wakiongozwa na LC 1 wa Chepskunya Chebet Siraji, wakazi hao walisema kwamba tatizo hilo linasababishwa pakubwa na watu kutoka jamii jirani ya karamoja na kwamba licha ya vikao vya kutafuta amani hamna hatua zozote ambazo zimepigwa.
Siraji sasa anataka kuandaliwe mkutano ambao utahudhuriwa na rais wa Uganda Yoweri Museveni ili kutafuta suluhu kwa tatizo hilo miongoni mwa jamii za Pokot, Sebei na Karamoja.
“Uhusiano kati ya jamii za Pokot na Sebei uko sawa ila kuna tatizo kwa upande wa Karamoja ambao wameendelea kuwa mwiba pande zote mbili, kwa wapokot na wasebei. Na kama viongozi tumejaribu kukaa ili kutatua swala hili ila hakuna suluhu hadi kufikia sasa.” Alisema Siraji.
Ni lalama ambazo pia zilitolewa na Monica Chepkough kiongozi kutoka eneo la Karita ambaye alisema kwamba wavamizi kutoka jamii hiyo wamepelekea mauaji ya wakazi wengi na kusababisha taharuki kubwa eneo hilo.
“Hawa watu wametuandama sana na mara nyingi wanakuja wakati wa usiku na kuwashambulia watu wakipora mali. Wameua watu wengi na sasa wamesababisha hali ya taharuki eneo hili hadi wengi wameanza kuhama makazi yao.” Alisema Chepkough.

[wp_radio_player]