JAMII MOJA NAKWIYEN YAHITAJI ZAIDI YA SHILINGI MILIONI 1 KWA UPASUAJI WA MOYO WA MWANAO.

Jamii moja eneo la Nakwiyen eneo bunge la Kacheliba katika kaunti ya Pokot magharibi inatoa wito kwa wahisani kujitokeza na kusaidia katika matibabu ya mwanao anayehitaji upasuaji wa moyo.

Kulingana na nyanyake Chemkan Cochena, Deborah Chepoisho mwanafunzi wa darasa la nane anahitaji zaidi ya shilingi mioni moja kufanyiwa upasuaji baada ya vipimo vilivyofanywa katika hospitali ya Kacheliba na kitale mtawalia kuonyesha uvimbe kwenye moyo wake.

Akizungumza alipotembelewa na wanahabari nyumbani kwake, Cochena alisema hawana uwezo wa kugharamia matibabu ya mtoto huyo kutokana na hali yao ya kifedha.

“Huyu mtoto alikuwa akilalamikia sana maumivu kwa moyo, na akifanya kazi kidogo tu anachoka sana. Tulimpeleka kufanyiwa uchunguzi kwenye hospitali za Kacheliba na Kitale ikabainika kwamba ana uvimbe anaohitaji kufanyiwa upasuaji. Tunahitaji shilingi milioni moja kufanikisha upasuaji huo. Tunaomba wahisani kutusaidia.” Alisema Cochena.

Wito huu ulikaririwa na mwalimu mkuu wa shule ya wasichana ya st. Paul Caron Dinah Lonyang’apoi anakosomea mwanafunzi huyo, na ambaye alisema hali hiyo imemfanya kutatizika kimasomo kuanzia mwezi januari mwaka huu ambapo hajakuwa akihudhuria masomo inavyohitajika.

“Deborah hajakuwa akihudhuria masomo inavyopasa kutokana na matatizo ya moyo. Alifikia hata kiwango cha kuwaaga wenzake kwamba hatarejea hali iliyonigusa sana. Naomba wote wanaoweza kusaidia katika kuchangisha fedha za kufanikisha upasuaji huo kujitokeza.” Alisema Lonyang’apoi.

Mwalimu wa mwanafunzi huyo Sarich Joseph alielezea wasi wasi kuhusu hatima ya masomo yake ikizingatiwa anafaa kufanya mtihani wa kitaifa wa darasa la nane KCPE mwaka huu.

“Tunaomba sana wahisani wamsaidie Deborah apate matibabu ili arejelee masomo yake kwa sababu ni mtahiniwa wa darasa la nane na hajasoma vizuri kwa sababu mara nyingi yuko kwenye matibabu, na dawa anazopewa ni za kutuliza tu maumivu.” Alisema Sarich.