JAMII KATIKA KAUNTI ZA POKOT MAGHARIBI, BARINGO NA ELGEYO MARAKWET ZATAKIWA KUJITENGA NA TAMADUNI YA UKEKETAJI.

Wito umetolewa kwa wakazi wa kaunti ya Pokot magharibi, Elgeyo marakwet na Baringo kujitenga na tamaduni za ukeketaji na badala yake kuangazia maswala ambayo yatapelekea jamii hizi kuafikia maendeleo na kujiimarisha kama jamii zingine.

Akizungumza eneo la Chesogon mpakani pa kaunti ya Pokot magharibi na kaunti jirani ya Elgeyo Marakwet, mwakilishi kina mama kaunt ya Elgeyo marakwet Carolyne Ng’elechei alisema kwamba jamii za kaunti hizi zimesalia nyuma kimaendeleo kwa kujihusisha na tamaduni ambazo zimepitwa na wakati.

Aidha Ng’elechei aliwataka wazazi kuwatunza vyema wanao wa kike msimu huu ambao huhusishwa na hafla nyingi, ili kuhakikisha kwamba wanarejea shuleni wakiwa katika hali nzuri kiafya, shule zitakapofunguliwa mwezi januari mwaka ujao.

“Kuna watu ambao bado wanajificha na kuketea wasichana. Nawaambia wakazi wa Pokot magharibi, Baringo na Elgeyo Marakwet kwamba hizi ni tamaduni ambazo zilipitwa na wakati. Tunapasa kuacha tamaduni hizi ili pia tusonge mbele kama jamii zingine.” Alisema Ng’elechei.

Wakati uo huo Ng’elechei aliwashauri wazazi kutoelekeza nguvu zote kwa mtoto wa kike na kumsahau mtoto wa kiume, badala yake kuhakikisha kwamba mtoto wa kiume pia anaangaziwa zaidi kwani  anakabiliwa na maswala yanayompa changamoto nyingi maishani ikiwemo utumizi wa mihadarati na kusajiliwa katika makundi ya kihalifu.

“Watoto wa kiume pia tuanapasa kuwalinda. Tusiegemee tu wale wa kike na kuwasahau wa kiume kwani pia wanakabiliwa na changamoto tele kama vile utumizi wa mihadarati pamoja na kusajiliwa katika makundi ya kihalifu ambayo yanaendeleza wizi wa mifugo maeneo haya.” Alisema.