ILANI YATOLEWA KWA WAKAZI WA TIATY KUSALIMISHA BUNDUKI YA POLISI.

Serikali imetoa makataa ya siku tatu kwa wakazi wa Ekoret eneo bunge la Tiati kaunti ya Baringo kurejesha bunduki ambayo inadaiwa kumilikiwa na mmoja wa maafisa wanane wa usalama waliouliwa katika eneo la Turkana mashariki.

Kamishna wa kaunti ndogo ya Tiaty jackton orieny amesema kufikia sasa wamefanikiwa kupata bunduki tano huku moja iliyosalia ikiaminika kufichwa katika eneo la akoret wakati ambapo oparesheni ya kutwaa silaha haramu mikononi mwa raia ikishika kasi kwa nia ya kurejesha amani katika eneo hilo.

Akiongea wakati wa mkutano uliowaleta wataalam, wazee na viongozi wa kidini kutoka jamii ya pokot, orieny alisema serikali haitasalia kimya tena huku wakazi wasio na hatia wakiendelea kuangamia mikononi mwa wahalifu na kulemaza shughuli za maendeleo

“Tunakwenda kukutana na hawa watu ana kwa ana tuwaulize ni kwa nini hawawezi kurudisha bunduki ya serikali kwa sababu bunduki ya serikali haiwezi kusalia mikononi mwa raia. Nawaonya watu wa Akoret kwamba wasijaribu kuondoa bunduki hiyo eneo ambako tunafahamu iko wakati huu.” Alisema Orieny.

Ni kauli ambayo imeungwa mkono na viongozi wa baringo kusini wakiongozwa na mbunge wa eneo hilo charles kamuren ambao wanaitaka serikali kuendeleza oparesheni hiyo kwa miaka miwili mfululizo ili kufanikisha zoezi la kutwaa bunduki zinazomilikiwa kinyume cha sheria na kuwapelekea wakazi waliokimbia makazi yao haswa katika maeneo ya kasiela, sinoni, arabal na kapindasum kurejea nyumbani.

“Tunaomba hiyo kazi iendelee. Na wasikwende tu kutafuta hiyo bunduki ya serikali ambayo ilichukuliwa bali waondoe bunduki zote ambazo zinamilikiwa na raia kwa sababu hata kufikia sasa shule zingine hazijafunguliwa kwa sababu ya utovu wa usalama.” Walisema.