IEBC YAWAHAKIKISHIA WAKENYA KUKAMILIKA MAANDALIZI YA UCHAGUZI MKUU.
Tume huru ya uchaguzi nchini IEBC imewahakikishia wakenya kuwa maandalizi yote yamekamilika kuelekea uchaguzi mkuu wa wiki ijayo.
Akizungumza katika mahojiano na kituo hiki afisa msimamizi wa uchaguzi wa tume hiyo katika kaunti ya Pokot magharibi Joyce Wamalwa, amesema kuwa vifaa vya kupigia kura vimesambazwa katika vituo vya kupigia kura maeneo bunge yote zikisalia karatasi za wadhifa wa urais pekee.
Wamalwa amewahakikishia wakazi wa kaunti ya Pokot magharibi kwamba usalama umeimarishwa kueleka uchaguzi huo.
“Kama tume tuko tayari sana kwa uchaguzi. Vifaa vyote ambavyo tunavihitaji kwa ajili ya tarehe 9 viko tayari na tumevisafirisha hadi kwa constituencies zetu.” Amesema Wamalwa.
Amesema tume hiyo ikishirikiana kikamilifu na idara ya usalama kuhakikisha kuwa shughuli hiyo inaendeshwa katika mazingira yaliyo salama.
“Ningependa kukuhakikishia kuwa usalama uko sawa. County Commander wetu na county commissioner, AP wetu wote wameweka mikakati ya kuhakikisha kwamba polling satations zetu ziko na usalama.” Amesema Wamalwa.
Wakati uo huo Wamalwa ameongeza kwamba, “katika kila kituo tutaruhusu ajenti mmoja kwa wakati. Na huyo ajenti ndiye atachunga kura. Kwa hivyo mtu akishapiga kura tafadhali tunawaomba waende nyumbani wakangoje matokeo.”
Taifa linaelekea katika uchaguzi mkuu juma lijalo tarehe 9 mwezi agosti, wawaniaji wa viti mbali mbali vya uongozi wakiwa katika awamu ya lala salama ya kampeni zao.