IEBC YATAKIWA KUWEKA MIKAKATI YA KUSAJILI WAPIGA KURA ZAIDI POKOT MAGHARIBI.
Zoezi la kuwasajili wapiga kura wapya likiingia leo siku ya tatu, viongozi katika kaunti hii ya Pokot magharibi wameendelea kuwahimiza wakazi kujitokeza kwa wingi ili kusajiliwa kuwa wapiga kura.
Seneta wa kaunti hii Samwel Poghisio amewahimiza wote ambao hawajasajiliwa kuhakikisha kuwa wanasajiliwa ili kuwa katika nafasi bora ya kutekeleza wajibu wao wa kidemokrasia wa kuwachagua viongozi wanaowapendelea katika uchaguzi mkuu wa mwezi agosti mwaka huu.
Wakati uo huo Poghisio amewataka maafisa wa tume ya uchaguzi IEBC wanaeondeleza shughuli ya kuwasajili wapiga kura kuweka mikakati ya kuwafikia wakazi wengi katika zoezi hilo ikiwemo kuwafuata waliko wafugaji waliohama makwao kutokana na ukame ili kuwasajili.
Kwa upande wake tume hiyo kupitia afisa wa usajili eneo la Pokot kusini Juma Mugwanga imesema kuwa imeweka mikakati ya kuhakikisha kuwa kila mmoja anafikiwa, ikiwemo kuwaajiri maafisa wa kutoa uhamasisho kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kusajiliwa kuwa wapiga kura.
Aidha Mugwanga amesema kuwa wanalenga kuwasajili wapiga kura alfu 30,868 idadi anayoelezea imani kuwa itaafikiwa shughuli nzima ya usajili wa wapiga kura itakapokamilika rasmi mwezi februari mwaka huu.