IEBC YATAKIWA KUTOA ELIMU YA UMMA KUHUSU VITUO VIPYA VYA KUPIGIA KURA.
Tume ya uchaguzi na uratibu wa mipaka IEBC imetakiwa kutoa elimu kwa umma kuhusiana na hatua ya tume hiyo kutaka kuongeza idadi ya vituo vya kupigia kura nchini.
Ni wito wake mwakilishi kina mama katika kaunti ya Trans nzoia Janet Nangabo ambaye amesema kuwa huenda baadhi ya wananchi wakakosa kufahamu kituo ambacho watatakiwa kupigia kura baada ya kuongezwa vituo hivyo hali inayopelekea ulazima wa elimu hiyo.
Aidha Nangabo ametaka kuwepo na maafisa zaidi wa IEBC ili kufanikisha shughuli ya upigaji kura bila changamoto zinazotokana na uchache wa maafisa hao.
Wakati uo huo Nangabo amewataka viongozi wa kisiasa ambao wanagombea viti mbali mbali katika uchaguzi mkuu wa mwezi agosti kuuza sera zao kwa njia ya amani na kutowagawa wananchi kwa misingi ya vyama na kikabila.