IDARA ZA USALAMA ZAENDELEA KUWEKA MIKAKATI YA KUKABILI VURUGU MAZISHINI BUNGOMA.


Idara za usalama maeneo mbali mbali katika kaunti ya Bungoma zimeendelea kuweka mikakati ya kuzuia vurugu katika hafla za mazishi ambazo zimetajwa kuchochewa pakubwa na viongozi wa kisiasa.
Akizungumza katika hafla moja ya mazishi eneo la Cheptais eneo bunge la mlima Elgon naibu chifu wa kata ndogo ya Ngachi Moses Chebus amedokeza mipango ya kupiga marufuku viongozi wa kisiasa kuhutubu katika hafla hizo ili kuzuia kushuhudiwa vurugu eneo hilo.
Chebus amesema kuwa baadhi ya viongozi wa kisiasa hutumia hafla za mazishi kutoa matamshi ya chuki dhidi ya viongozi wengine, akisema huenda akalazimika kuwanyima fursa ya kuhutubu kwenye hafla hizo.
Wakati uo huo Chebus amesema kuwa mikakati inaendelea kuwekwa kudumisha amani eneo hilo ambalo kwa wakati mmoja lilikithiri utovu wa usalama, akisema kuwa wote waliohusika uhalifu eneo hilo lazima watakabiliwa kisheria.