IDARA ZA USALAMA NA ELIMU POKOT MAGHARIBI ZAENDELEZA MIKAKATI YA KUKABILI MIOTO SHULENI.

Na Benson Aswani

Mikakati inaendelea kuwekwa na idara za usalama kwa ushirikiano na ile ya elimu kuhakikisha kuwa visa vya mioto shuleni ambavyo vimeonekana kuongezeka katika siku za hivi karibuni nchini vinathibitiwa.
Akizungumza katika kikao na wanafunzi wa shule ya upili ya wavulana ya Ortum kaunti hii ya Pokot magharibi, naibu kamishina eneo la Kipkomo Teresa Moguro hata hivyo amewataka wanafunzi kutumia muda wao vizuri shuleni na kutojihusisha na maswala ambayo huenda yakawapelekea kujutia katika maisha yao ya baadaye.
Moguro amewataka wanafunzi kutumia mbinu zinazokubaliwa kusuluhisha matatizo ambayo wanahisi kukabiliana nayo shuleni wakiwemo walimu akisema kuwa ni jukumu lao kuhakikisha usalama wa vifaa na mali za shule.
Ni kauli ambayo imesisitizwa na mkurugenzi wa elimu kaunti hii ya Pokot magharibi Evans Onyancha ambaye pia amesema kuwa afisi yake itashughulikia baadhi ya malalmishi ambayo yametolewa na wanafunzi hao japo akiwasisitizia haja ya kutumia kwanza raslimali zilizopo.
Yanajiri haya huku wanafunzi watatu wa shule ya upili ya Ortum katika kaunti hii ya Pokot magharibi wakitarajiwa leo kufikishwa mahakamani katika mahakama ya kapenguria baada ya kukamatwa hiyo jana kwa tuhuma za kuteketeza bweni la shule hiyo.