IDARA ZA USAJILI KACHELIBA ZASHUTUMIWA KWA KUWAHANGAISHA WAKAZI.
Mkazi mmoja kutoka Eneo la Kacheliba kaunti hii ya pokot magharibi anatoa wito wa kuingiliwa kati idara husika kwa kile amedai kuhangaishwa na ofisi za chifu na ya usajili vyeti vya kuzaliwa pamoja na vya kitaifa kutokana na kile amedai ni ukabila na ubaguzi wa kidini.
Kulingana na Mama huyo ambaye hakutaka jina lake kutajwa, juhudi zake kupata cheti cha kuzaliwa pamoja na kitambulisho cha kitaifa kwa mwanawe mwenye umri wa miaka 21 zimekuwa zikiambulia patupu na kuwa haambiwi lilipo tatizo na maafisa husika.
Aidha mama huyo anadai huenda mahangaiko yake yanatokana na hali kuwa hana mme baada ya kutofautiana na mmewe hali iliyopelekea wao kutengana huku akitoa wito kwa serikali kuhakikisha kuwa haki za wajane na wazazi wa kike waliotengana na waume wao zinalindwa.