IDARA ZA UCHUNGUZI ZATAKIWA KUCHUNGUZA KUPORWA FEDHA ZA CHAM CHA USHIRIKA KACHELIBA

Wanachama wa chama kimoja cha ushirika eneo la Kacheliba katika kaunti hii ya Pokot magharibi wanalilia haki baada ya kuporwa fedha zao na wanaodaiwa kuwa viongozi wa chama hicho wakitaka idara ya uchunguzi DCI kuendeleza uchunguzi kuhusu hali hiyo.

Wakiongozwa na Pamela Chenang’at wanachama hao wanasema kuwa walibuni chama hicho cha ushirika kuhifadhi fedha walizokuwa wakipokea kutoka kwa mradi wa huduma kwa vijana NYS ila sasa kiasi kikubwa fedha kimetolewa katika akaunti yao kwa njia isiyoeleweka.

Aidha wanachama hao wamemshutumu mwakilishi wadi wa eneo hilo kwa madai ya kuwalipia bondi baadhi ya viongozi wa chama hicho waliokamatwa kwa kuhusika wizi wa fedha hizo wakimtaka kujitokeza wazi kuelezea sababu ya kuchukua hatua hiyo.

Ni kauli ambayo imetiliwa mkazo na aliyekuwa msimamizi wa vijana hao kwenye mradi huo Mustapha Oketal ambaye amesema walihifadhi zaidi ya shilingi milioni 34 kinyume walizokabidhiwa wakitaka idara za kukabili ufisadi kuingilia kati.