IDARA YA USALAMA POKOT YA KATI YAKANA KUTUMIA NGUVU KUPITA KIASI KATIKA OPARESHENI ZA KIUSALAMA.

Idara ya usalama eneo la Pokot ya kati katika kaunti ya Pokot magharibi imepuuzilia mbali madai kwamba inatumia nguvu kupita kiasi wakati inapoendeleza oparesheni ya kukabili wahalifu ambao wanasababisha utovu wa usalama maeneo ya mipakani pa kaunti hiyo.

Akirejelea oparesheni iliyoendeshwa eneo la Cheptulel eneo bunge la sigor ambapo maafisa wa polisi walilaumiwa kwa madai ya kuwahangaisha wananchi, naibu kamishina eneo hilo Jeremiah Tumo alisema kwamba oparesheni hiyo hailengi kwa vyovyote wananchi bali ni wahalifu ambao wanadaiwa kujificha miongoni mwa wananchi.

“Oparesheni ambayo inaendelea maeneo ya mipakani pa kaunti za bonde la kerio hailengi kwa vyovyote wananchi wa kawaida. Tunalenga wahalifu. Maafisa wetu wanatumia taarifa za kijasusi na iwapo watapata taarifa kwamba kuna mhalifu sehemu yoyote watafanya msako eneo hilo kuhakikisha kwamba mhalifu anaondolewa miongoni mwa wananchi.” Alisema Tumo.

Tumo alitoa wito kwa wakazi wa vijiji vilivyoathirika na oparesheni hiyo ya wiki jana na ambao walihama kwa kuhofia kuhangaishwa na maafisa wa polisi, kutokuwa na hofu na kurejea ili kuwasaidia maafisa hao kuhakikisha wahalifu wanakabiliwa akisema mipango ya serikali itaathirika pakubwa iwapo wataghura maeneo hayo.

“Tunawataka wakazi wa maeneo husika ambao walihama kufuatia oparesheni hiyo kurejea nyumbani ili tuweze kuendelea nao pamoja kwa zile kazi tulizokuwa tukifanya, kwa sababu iwapo hawatakuwepo basi itakuwa vigumu kwetu kutekeleza mipango ya serikali hasa kusambaza chakula cha msaada.” Alisema.

Hata hivyo, Tumo alisema kwamba oparesheni ya maafisa wa usalama ambayo imekuwa ikiendelea eneo hilo imesaidia pakubwa kupunguza kwa asilimia 60 visa vya wizi wa mifugo ambavyo vimekuwa vikiripotiwa.

“Tangu oparesheni hiyo kuanza tumefanikiwa pakubwa. Visa vya wizi wa mifugo vimepungua kwa asilimia 60. Hapo awali tulikuwa tukiripoti visa kama vinne kwa wiki, ila sasa tunaweza kuripoti visa kama vitatu hivi kwa mwezi.” Alisema.