IDARA YA USALAMA POKOT MAGHARIBI YAWAHAKIKISHIA WATAHINIWA MAZINGIRA SALAMA KIPINDI CHA MITIHANI.

Idara ya usalama katika kaunti ya Pokot magharibi imeendelea kuwahakikishia watahiniwa wa mtihani wa kitaifa kwa kidato cha nne KCSE ambao umeingia siku yake ya pili kwamba hali ya usalama imeimarishwa ili kuwapa mazingira bora ya kufanya mtihani huo.

Kamanda wa polisi eneo la Kapenguria Joel Kirui alisema kwamba kila kituo cha mtihani eneo hilo kinalindwa na maafisa wawili wa usalama huku vituo vya mitihani vilivyo maeneo ambayo yamekuwa yakishuhudia utovu wa usalama hasa maeneo ya mipakani vikilindwa na maafisa wa jeshi.

Aidha Kirui alisema kwamba idara ya polisi imetoa magari ambayo yanawasindikiza maafisa wa elimu wanaosafirisha karatasi za mitihani hadi katika vituo mbali mbali vya kufanyia mitihani hiyo.

“Kwa upande wa usalama tumejipanga vilivyo kuhakikisha kwamba wanafunzi wanafanya mtihani wao katika mazingira salama. Kila kituo cha mtihani kimelindwa na maafisa wawili wa polisi huku shule zilizo maeneo ambayo yanakumbwa na utovu wa usalama zikilindwa na maafisa wa jeshi.” Alisema Kirui.

Wakati uo huo Kirui alisema idara ya polisi inashirikiana na idara ya elimu kuhakikisha kwamba hakushuhudiwi ugumu wa kusafirisha karatasi za mitihani hasa katika maeneo ambayo yanakabiliwa na changamoto za usafiri kufuatia mvua inayoendelea kushuhudiwa.

“Kuna sehemu zingine ambazo ni vigumu kwa magari kupita kufuatia mvua inayoendelea kushuhudiwa. Idara ya usalama itashirikiana kikamilifu na ya elimu kuhakikisha kwamba tatizo hili linashughulikiwa ikiwemo kutumia ndege kusafirisha makaratasi ya mtihani.” Alisema.