IDARA YA USALAMA POKOT MAGHARIBI YATAKIWA KUWAJIBIKA NA KUWAKABILI WAHALIFU MAKUTANO.

Naibu gavana wa kaunti hii ya Pokot magharibi Robert Komole ameitaka idara ya usalama katika kaunti hii kushirikiana na viongozi katika kuhakikisha kwamba usalama wa wakazi wa kaunti hii unaimarishwa.

Komole alisema kwamba hali ya utovu wa usalama imeripotiwa kuongezeka hasa mjini Makutano, akimtaka kamishina wa kaunti hiyo Apolo Okelo kuhakikisha kwamba maafisa wa usalama wanaendesha doria ili kuhakikisha wanaoendeleza uovu huo wanakabiliwa.

“Kuna watu ambao wanaendeleza uhalifu katika mji wa makutano. Tumepokea ripoti za akina mama kubakwa na sasa hali ya usalama imekuwa tete katika mji huu. Tunataka kamishina wa kaunti hii kuhakikisha kwamba kuna doria inayoendeshwa na maafisa wa usalama kukabili uovu huu hasa nyakati za usiku.” Alisema Komole

Aidha Komole alimtaka kamshina huyo kufanya uchunguzi kuhusiana na habari za uongo ambazo zinaenezwa na baadhi ya wakazi kwamba mifugo wameaga dunia kufuatia chanjo ambayo imetolewa na gavana wa kaunti hiyo hali ambayo imehujumu shughuli hiyo kufuatia hofu ambayo imewekwa kwa wakazi.

“Kuna watu ambao wanaeneza madai ya uongo kwamba chanjo ambayo inatolewa na gavana kwa mifugo si salama na imepelekea mifugo wengi kuaga dunia. Na hawa watu wako tu. Tunamtaka kamishina wa kaunti hii kuendesha uchunguzi kuhusu wanaoeneza madai haya ili wachukuliwe hatua kwa sababu sasa wamewatia hofu wakazi wengi.” Alisema.

Wakati uo huo Komole alisisitiza marufuku iliyowekwa na kamishina wa kaunti hiyo kwa sherehe za nyakati za usiku, akiwataka machifu kuhakikisha kwamba hakushuhudiwi sherehe hizo maeneo yao ya uwakilishi kama njia moja ya kuzuia mimba za mapema.