IDARA YA USALAMA POKOT KUSINI YALENGA KUPIGA MARUFUKU BIASHARA YA POMBE NA MICHEZO YA ‘POOL’.
Na Emmanuel Oyasi.
Idara ya usalama eneo la pokot kusini kaunti ya Pokot magharibi inaendeleza vikao vya kutafuta maoni ya wakazi wa eneo hilo kuhusu biashara ya pombe na michezo ya pool kabla ya kuweka mikakati ya kukabili biashara hiyo eneo hilo.
Akizungumza baada ya kuandaa kikao na wakazi wa eneo la Kabichbich, naibu kamishina eneo hilo David Bowen alisema kwamba wengi wa wakazi wamepinga biashara hiyo na kwamba idara ya usalama itatekeleza maoni hayo ya wananchi.
“Tunaandaa vikao na wananchi sehemu hii ili kupata maoni yao kuhusu biashara ya pombe na michezo ya pool. Wananchi wana matakwa yao na sisi kama maafisa wa usalama tutatekeleza yale ambayo wananchi watasema.” Alisema Bowen.
Kauli yake ilisisitizwa na kamanda wa polisi eneo hilo Seth Sudi ambaye alisema kwamba biashara hizi zimekuwa zikipelekea ongezeko la utovu wa usalama, na msimamo huo wa wananchi sasa utawapa fursa ya kuhakikisha kwamba zinakabiliwa.
“Kuna swala la utovu wa usalama ambao huambatana na biashara ya pombe na michezo hii ya pool, kwa sababu watoto hawa wametoka shule majuzi, wanawaibia wazazi wao ili waende wacheze pool. Tunaona wengi wa wakazi wanakataa biashara hii na sisi tufanya kile wanachotaka.” Alisema Sudi.
Ni hatua ambayo iliungwa mkono na wakazi wa eneo hilo ambao walihudhuria kikao hicho wakisema biashara hizo zimepelekea vijana wengi kupotoka maadili.