IDARA YA POLISI POKOT MAGHARIBI YAENDELEZA MSAKO WA WAHALIFU WALIOWAUA WATU WATATU KAPLON.
Kamanda wa polisi kaunti ya Pokot magharibi Peter Katama ameshutumu vikali mauaji ya watu watatu wakazi wa eneo la Kaplon pokot kaskazini, mauaji ambayo yanakisiwa kutekelezwa na wahalifu wanaoaminika kutoka kaunti jirani.
Akizungumza na kituo hiki Katam alisema kwamba maafisa wa polisi wanaendeleleza msako wa wahalifu hao ambao walitoweka baada ya kutekeleza mauaji hayo, akiahidi kushirikiana na wakazi kuhakikisha kwamba wahalifu wote wanakabiliwa.
“Watu watatu waliuliwa kwa risasi na majangili kutoka kaunti jirani eneo la Kaplon. Tunalaani sana kisa hicho na nawahakikishia wakazi wa eneo hilo kwamba tunafanya kila juhudi kuhakikisha majangili hawa wanapatikana na kuchukuliwa hatua.” Alisema Katam.
Aidha Katama aliwahimiza wakazi wanaoishi eneo hilo na maeneo mengine ambayo yamekuwa na historia ya utovu wa usalama kudumisha amani, akitumia fursa hiyo pia kuwahakikishia watahiniwa kwamba usalama umedumishwa kuhakikisha wanafanyia mitihani yao katika mazingira salama.
“Nawahimiza wakazi wa maeneo ambayo yanakabiliwa na utovu wa usalama kwamba tudumishe amani, tusiwe na tamaa ya kuchukua sheria mkononi. Nawahakikishia pia wanafunzi ambao wanafanya mtihani kwamba, kuna maafisa wa kutosha wa usalama kuhakikisha wanafanya mitihani yao katika mazingira salama.” Alisema.
Kauli yake Katam inajiri wakati wakazi maeneo mbali mbali ya kaunti hiyo wakiongozwa na mwenyekiti wa baraza la wazee eneo la pokot kusini Mastayit Lokales wakiendelea kushinikiza serikali kuwaajiri na kuwakabidhi bunduki maafisa wa NPR kaunti hiyo ili kudumisha usalama.
“Naiambia serikali kwamba iwapo kaunti ya Pokot haitapata maafisa wa NPR na kukabidhiwa bunduki, basi iwapokonye maafisa hao silaha katika kaunti za Turkana na Elgeyo marakwet kwa sababu hizo silaha ndizo zinazotumika kuendeleza uhalifu maeneo haya.” Alisema Lokales.