IDARA YA POLISI POKOT MAGHARIBI YAAPA KUKABILIANA NA WALANGUZI WA RISASI.

Kamanda wa polisi kaunti ya Pokot magharibi Peter Katam amewahakikishia wakazi wa kaunti hiyo kwamba idara ya polisi imeweka mikakati ya kuhakikisha  wafanyibiashara waneoendeleza biashara haramu ya uuzaji risasi wanakabiliwa.

Akirejelea kisa cha jumanne ambapo mafisa wa polisi walinasa risasi 749 zilizokuwa zikisafirishwa na mhudumu wa boda boda eneo la Marich, Katam alisema kwamba wakazi wengi ikiwemo maafisa wa usalama wameuliwa na wahalifu na kamwe hawataruhusu biashara hii kuendelezwa.

Alitoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na maafisa wa polisi kwa kutoa taarifa kuhusu visa vyovyote ambavyo huenda vikapelekea utovu wa usalama ili kuhakikisha kwamba wahusika wanakabiliwa.

“Hawa wafanyibiashara wa kuuza risasi siku zao zimefika mwisho kwa sababu tumeziba mianya yote ambayo ilikuwa inaruhusu kuendelezwa biashara hiyo. Tumeshuhudia visa ambapo maafisa wa polisi na raia wameuliwa na wahalifu, hivyo tunawasihi wananchi tuendelee kushirikiana katika vita hivi.” Alisema Katam.

 Wakati uo huo Katam aliwapongeza maafisa wa polisi ambao walinasa risasi hizo alizosema kwamba huenda zingesababisha maafa zaidi iwapo zingefika mikononi mwa wahalifu. 

“Iwapo hizi risasi zingefika mikononi mwa wahalifu tungeshuhudia maafa mengi. Kwa hivyo nawapongeza maafisa walionasa risasi hizi na nawahimiza kuendeleza doria ili kuhakikisha wahalifu hawapati nafasi ya kuendeleza vitendo vyao vya kihalifu.” Alisema.