IDARA YA POLISI KACHELIBA YAPIGA MARUFUKU DENSI ZA USIKU.

Idara ya polisi eneo la kacheliba kaunti ya Pokot magharibi imepiga marufuku hafla zozote za usiku katika eneo hilo hasa msimu huu wa desemba ambao huandamana na sherehe nyingi.

Akizungumza na kituo hiki, OCS wa eneo hilo Tom Nyanaro alisema kwamba hafla hizo huambatana na maovu mengi ambayo hupelekea mimba na ndoa za mapema miongoni mwa watoto wa kike ambao huishia kukatiza masomo yao.

Aidha Nyanaro alisema kwamba hafla hizo pia hutumika kupanga jinsi ya kuwakeketa watoto wa kike akionya kwamba hatua kali za sheria zitachukuliwa dhidi ya watakaopatikana wakiendeleza hafla hizo.

“Tumepiga marufuku hafla za usiku na watakaopatikana watachukuliwa hatua za kisheria. Hafla hizi zimechangia watoto wengi wa shule kupachikwa mimba na hata wengine kuolewa mapema hali ambayo imewapelekea wengi kusitisha masomo.” Alisema Nyanaro.

Nyanaro aliwataka wazazi kutekeleza majukumu yao ya ulezi na kuhakikisha kwamba wanao wanalindwa vyema hasa katika likizo hii ndefu huku pia akiwahimiza viongozi wa kidini kuchangia katika kukabili uovu huo kwa kuwapa wakazi mwelekeo.

“Jukumu la kwanza kwa wazazi ni kuwalinda watoto wao hata kabla ya serikali kuja kuwalinda. Nawaonya wazazi kuchukua tahadhari. Nawataka pia viongozi wa kidini kutusaidia katika maswala haya kwa kuwapa mwelekeo wananchi.” Alisema.