Idara ya elimu Pokot magharibi yalaumiwa kwa changamoto zinazoshuhudiwa

Na Emmanuel Oyasi,
Mbunge wa Kapenguria Samwel Moroto ameusuta uongozi wa elimu katika kaunti ya Pokot magharibi kwa kususia hafla muhimu ambazo zinahusu maswala ya elimu.
Akizungumza wakati akizundua fedha za basari katika shule ya wasichana ya Kamito, Moroto alisema zipo changamoto tele zinazoshuhudiwa katika sekta ya elimu, ambazo zinafaa kuangaziwa na idara ya elimu ila maafisa wake wamekuwa wakisusia hafla wanazofaa kutumia kuangazia changamoto hizo.
“kuna shida katika sekta ya elimu kaunti hii na maafisa wa elimu hawajitokezi katika hafla muhimu kama hizi kuelezea kinachofanyika kwenye sekta hiyo,” alisema Moroto.
Alisema wakuu wa idara ya elimu kaunti hiyo wanafaa kujukumika na kushughulikia matatizo ambayo yanakumba shule nyingi na kupelekea migomo ya kila mara.
Viongozi waliohudhuria hafla hiyo akiwemo mbunge wa Sigor Peter Lochakapong walitetea hazina ya CDF wakisema kwamba imekuwa na manufaa makubwa kwa wanafunzi kutoka jamii zenye changamoto za kifedha.
“Fedha za CDF zimesaidia sana wananchi kupitia ujenzi wa shule na hata kupitia basari. Watu wana ushuhuda kamili kwamba fedha hizo zimekuwa na manufaa. Kwa hivyo wale ambao wana mawazo ya kuondoa CDF, wafikirie tena,” alisema Lochakapong.
Kauli za viongozi hao zilitiliwa mkazo na mwalimu mkuu wa shule hiyo Francisco Diku ambaye alielezea manufaa ya fedha hizo kwa shule yake hasa ikizingatiwa ina wanafunzi wengi wenye mahitaji maalum.
“Wanafunzi wengi wanatoka katika familia zenye changamoto kubwa ya kifedha na wakati mwingine wakitumwa nyumbani kutafuta karo hawarudi. Na sasa kwa kuwa fedha za basari zimezinduliwa, najua zitakuwa za msaada sana kwa wengi wao,” alisema Bi. Diku.
Moroto alizindua basari ya kima cha shilingi milioni 58.