IDARA YA AFYA TRANS NZOIA YALENGA KUIMARISHA UTOAJI CHANJO YA COVID 19.

Na Benson Aswani
Idara ya afya Kaunti ya Trans-Nzoia imeandaa mikutano na washikadau kutoka sekta mbalimbali kama njia moja ya kuimarisha kampeni ya utoaji wa chanjo dhidi ya covid 19 ili kuafikia lengo la kitaifa la kuchanja zaidi ya watu Milioni 10 kote nchini mwishoni mwa mwaka huu.
Kwa mujibu wa afisa wa uhamasishaji wa maswala ya afya Kaunti ya Trans-Nzoia Leah Okumu awamu ya kwanza ya chanjo hiyo ililenga wahudumu wa afya, maafisa wa usalama na wanaoishi na magonjwa sugu,huku awamu ya sasa ikilenga akina mama wajawazito na wanaonyonyesha pamoja na waliotimu umri wa miaka 18 na zaidi.
Aidha Okumu amesema wizara ya afya Kaunti hiyo imebuni maeneo 56 ya kutoa chanjo hiyo mashinani kando na vituo 36 vya afya kaunti hiyo vinavyotoa chanjo hiyo, akisema awamu ya tatu ya chanjo hiyo inalenga kuafikia asilimia 60% ya watu kote nchini ifikiapo mwisho wa mwaka wa 2022, akionya umma dhidi ya kutozingatia masharti ya wizara ya afya baada ya kupokea chanjo hiyo.