IDARA MBALI MBALI ZA SERIKALI YA POKOT MAGHARIBI ZAWASILISHA RIPOTI ZA MAONI KUHUSU MAANDALIZI YA BAJETI.
Waakilishi wadi katika kaunti ya Pokot magharibi wamewahakikishia wananchi kwamba watafuatilia kwa karibu kuhakikisha kwamba maoni yaliyotolewa kuhusu utekelezwaji wa bajeti yanatekelezwa kikamilifu.
Akizungumza wakati wa vikao vya kuangazia ripoti kutoka idara mbali mbali kuhusiana na maoni yaliyotolewa na wananchi katika shughuli ya kuwahusisha kabla ya kuandaa bajeti, viongozi hao wakiongozwa na kiongozi wa wengi katika bunge hilo Martine Komongiro walisema watahakikisha katiba inazigatiwa kikamilifu.
“Sisi katika serikali hii ikiongozwa na gavana Simon Kachapin tunasimamia katiba, kwamba nguvu inatokana na wananchi. Hivyo tutafuatilia hadi mwisho kile wananchi walisema katika vikao vya maoni ili matakwa yao yazingatiwe kikamilifu.” Alisema Komongiro.
Viongozi hao walisema kwamba ripoti hizo zitaangaziwa kulingana na maswala ambayo yalipewa kipau mbele na wananchi wakati wa vikao hivyo, kuhakikisha kwamba bajeti itakayoundwa inaangazia pakubwa matakwa ya wananchi.
“Tunafuatilia kuona yale ambayo waliyapa kipau mbele katika kila idara ili yazingatiwe wakati wa kutengeza bajeti.” Walisema.
Waziri wa fedha na mipango ya uchumi katika kaunti hiyo Priscilla Chebet alisema kwamba serikali inafanya kazi kwa karibu na wabunge katika bunge la kaunti kuhakikisha mabadiliko yatakayofanyika katika ripoti hizo hayataathiri mipango ya kuandaa bajeti.
“Kama serikali ya kaunti tumeamua kutembea pamoja na bunge la kaunti ili kuhakikisha kwamba hakuna mabadiliko mengi ambayo yatafanyika katika hatua ya bunge na kuathiri maandalizi ya bajeti.” Alisema Chebet.