IDADI KUBWA YA WANAFUNZI YAPELEKEA UHABA WA MIUNDO MSINGI SHULENI.

Shule mbali mbali za upili katika kaunti ya Pokot magharibi zimeendelea kukabiliwa na uhaba wa miundo msingi kufuatia idadi kubwa ya wanafunzi wa kidato cha kwanza ambao walisajiliwa katika shule hizo kufuatia sera ya serikali ya mpito wa asilimia 100.

Wa hivi punde kulalamikia hali hiyo ni mwalimu mkuu wa shule ya upili ya wasichana ya Chester Bi. Patricia Nandi, ambaye alisema kwamba shule hiyo imepokea jumla ya wanafunzi 310 kufikia sasa ambapo wanafunzi zaidi wanaendelea kuwasili.

Bi. Nandi alisema shule hiyo inakabiliwa na upungufu wa madarasa matatu ambapo kwa sasa baadhi ya wanafaunzi wanalazimika kuendeleza masomo yao chini ya mti, huku wengine wakisomea katika chumba cha mankuli, mabweni yakiwa pia changamoto ambapo wanafunzi 917 wanalazimika kulala kwenye bweni lenye uwezo wa kukimu wanafunzi 480.

“Mwaka huu tumepokea wanafunzi 310 ambao wamejiunga na kidato cha kwanza na bado wanawasili. Hivyo tunashuhudia upungufu wa madarasa kama matatu hivi ambapo baadhi ya wanafunzi wanasomea chini ya mti. Pia tunahitaji bweni, kwa sababu bweni lililopo lina uwezo wa kukimu wanafunzi 480 lakini sasa wanafunzi 917 wanalazimika kulala kwenye bweni hilo.” Alisema Nandi.

Aidha Bi. Nandi alisema kwamba wanapitia changamoto kuu kupata maji ambapo wanayopata kwa sasa hayatoshelezi mahitaji ya shule hiyo, akitoa wito kwa wahisani kujitokeza na kusaidia kuimarisha hali katika shule hiyo ili kutoa mazingira bora kwa wanafunzi kuendeleza shughuli za masomo bila ya changamoto.

“Tunaomba wahisani kujitokeza na kutujengea madarasa na bweni pamoja na kutuchimbia kisima ambapo tutakuwa tukipata maji, kwa sababu tunapata changamoto pia kwani tunayopokea kwa sasa hayatoshelezi mahitaji ya shule.” Alisema.