HUENDA UKOSEFU WA MVUA KATIKA KAUNTI YA POKOT MAGHARIBI UKAATHIRI MAVUNO MWAKA HUU
Serikali ya taifa imetakiwa kuanza mipango ya kuweka mikakati ya kuwasaidia wakazi wa maeneo mengi ya kaunti hii ya Pokot Magharibi kwa chakula katika siku za usoni.
Ni wito wake mwakilishi wadi maalum eneo la Masol Grace Rengei ambaye amesema kuwa wakazi wengi hawatakuwa na mavuno ya kutosha mwaka huu kutokana na uchache wa mvua hali ambayo imesababisha mimea ya wakazi wengi kunyauka.
Wakati uo huo Rengei ameshutumu kile ametaja siasa mbovu katika kaunti hii ambazo zilivuruga mpango wa serikali ya kaunti hii ya Pokot Magharibi kutoa msaada wa chakula kwa wakazi huku akimhimiza gavana John Lonyangapuo kutokata tamaa na badala yake kuendelea kuwasaidia wakazi wanaokabiliwa na hali ngumu ya maisha.