HUDUMA ZA MATIBABU ZATARAJIWA KUIMARIKA KASEI BAADA YA KUFUNGULIWA ZAHANATI MBALI MBALI.

Waziri wa afya katika kaunti hii ya Pokot magharibi Cleah Parklea ametaja hatua ya kufunguliwa zahanati maeneo ya Chepelion, Lelmelo, Kamketo na Opol kuwa ya muhimu zaidi katika kuhakikisha huduma bora za matibabu kwa wakazi wa kaunti  ya Pokot magharibi.

Akizungumza eneo la Kasei, Parklea alisema kwamba hatua hiyo itasaidia pakubwa kupunguza msongamano wa wagonjwa katika hospitali ya rufaa ya Kapenguria kwani magonjwa ambayo yanaweza kushughulikiwa katika ngazi za chini yatashughulikiwa kwenye zahanati hizo.

Aidha Parklea alisema hatua hiyo itaiwezesha hospitali ya Kapenguria kushughulikia tu magonjwa sugu ambayo hayawezi kushughulikiwa kwenye zahanati hizo.

“Kwa kufungua hizi zahanati tumepunguza pakubwa msongamano katika hospitali ya rufaa ya Kapenguria. Magonjwa mengi yanahudumiwa katika zahanati hizi isipokuwa tu yale ambayo ni sugu, ndiyo yanayoelekezwa katika hospitali ya Kapenguria.” Alisema Parklea.

Ni hatua ambayo pia ilipongezwa na chifu wa Kasei Elijah Mengich ambaye alisema kwamba kwa miaka mingi wakazi wa eneo hilo wamekuwa wakipitia wakati mgumu kupata huduma za afya kutokana na ukosefu wa vituo vya kutoa huduma hizo eneo hilo.

“Kwa miaka mingi wakazi wa eneo hili wamekuwa wakihangaika kupata huduma za matibabu kutokana na ukosefu wa vituo vya afya eneo hili la Kasei. Lakini sasa tutapata huduma hizi bila tatizo baada ya zahanati hizi kufunguliwa.” Alisema Mengich.