HUDUMA ZA MAHAKAMA ZATARAJIWA KUIMARIKA POKOT MAGHARIBI IDARA HIYO IKILENGA KUJENGA MAHAKAMA ZAIDI.


Idara ya mahakama kwa ushirikiano na serikali ya kaunti ya Pokot magharibi inalenga kufungua mahakama zingine mbili maeneo ya Alale na Sigor kama njia moja ya kupeleka huduma za mahakama karibu na mwananchi.
Akizungumza baada ya kufanya kikao na gavana Simon Kachapin, jaji wa mahakama kuu ya Kitale na ambaye pia anahudumu katika mahakama ya Kapenguria Anthony Mrima alisema kwamba lengo la hatua hiyo ni kupunguzia wakazi wa maeneo hayo gharama ya kusafiri hadi kapenguria kutafuta huduma za mahakama.
“Tumekubaliana kwamba tutafute fedha ili tujenge koti kule maeneo ya Alale na Sigor na kwingineko ili watu wetu wasitumie muda mrefu na gharama nyingi kufika Kapenguria ili kupata huduma za mahakama.” Alisema Mrima.
Wakati uo huo Mrima aliwahakikishia wakazi wa kaunti ya Pokot magharibi walio na kesi mahakamani kwamba atahakikisha kesi zao zinashughulikiwa na kukamilika kwa wakati ili wahusika watendewe haki haraka iwezekanavyo.
“Nawataka wakazi wa kaunti hii kutokuwa na wasiwasi. Nawaahidi kwamba kesi ambazo ziko katika mahakama kuu zitapelekwa vizuri na kuhakikisha kwamba wahusika wanatendewa haki haraka iwezekanavyo.” Alisema.
Kwa upande wake gavana Simon Kachapin alitoa wito kwa serikali ya kitaifa kuongeza mgao wa idara ya mahakama ili kuiwezesha kufanikisha juhudi za kuhakikisha kwamba inapeleka huduma zake karibu na mwananchi kwa kujenga mahakama zaidi.
“Natoa wito kwa serikali kuu indelee kuongeza mgao wa bajeti kwa idara ya mahakama ili waendeshe kazi yao kwa njia inayofaa na kufanikisha juhudi za kuhakikisha kwamba huduma za mahakama zinamfikia mwananchi kwa ukaribu.” Alisema Kachapin.
Wakati uo huo Kachapin alitoa wito kwa wakazi wa kaunti hiyo kukumbatia mbinu mbadala za kusuluhisha mizozo ikiwemo matumizi ya wazee wa mitaa ili kuzuia mirundiko ya kesi mahakamani.
“Iwapo kuna kesi ambazio zinaweza kutatuliwa kwa njia mbadala itakuwa bora ili kuzuia mirundiko ya kesi mahakamani. Naomba wakazi wakumbatie njia za kutumia wazee wa mitaa kutatua baadhi ya kesi kwa mfano zinazohusu maswala ya ardhi.” Alisema.

[wp_radio_player]