HOSPITALI YA RUFAA YA KAPENGURIA YAIMARISHA HUDUMA ZA UPASUAJI.

Hospitali ya rufaa ya Kapenguria.


Na Benson Aswani.
Hospitali ya Kapenguria katika kaunti ya Pokot magharibi imeendelea kuweka mikakati ya kuimarisha huduma kwa wagonjwa wanaohitaji upasuaji.
Kulingana na mkuu wa matibabu katika hospitali hiyo Dkt Simon Kapchanga, hospitali hiyo inaendeleza mikakati hiyo kupitia kufadhili masomo zaidi kwa baadhi ya madaktari ambao watakuwa wanatoa huduma hizo, upasuaji wa ubongo ukipewa kipau mbele.
Akizungumza afisini mwake, Kapchanga alisema kwamba tayari huduma hizo zinatolewa katika hospitali hiyo ikiwa ya pekee eneo hili kutoa huduma za upasuaji wa ubongo na uti wa mgongo, kando na hospitali ya rufaa na mfunzo ya Moi mjini Eldoret.
“Tumewatuma madaktari wetu kupata ujuzi zaidi hasa kuhusiana na magonjwa ambayo yanahitaji upasuaji. Mmoja wetu amemaliza masomo ya upasuaji wa ubongo ambapo anasaidia sana katika huduma hizi kwenye hospitali hii. Hii ni hospitali ya pekee eneo hili inayotoa huduma za upasuaji wa ubongo kando na ile ya MTRH mjini Eldoret.” Alisema Kapchanga.
Dkt. Kapchanga alisema visa kadhaa vinavyohitaji upasuaji wa ubongo vimeshughulikiwa katika hospitali hiyo matokeo yakiwa ya kuridhisha, hali ambayo imefanya hospitali ya Kapenguria kupokea wagonjwa wanaohitaji huduma hizo kutoka hata kaunti jirani.
“Awali tulikuwa tukiwatuma wagonjwa wanaohitaji upasuaji wa ubongo katika hospitali ya MTRH. Lakini sasa tunatoa matibabu hayo na hata wagonjwa wanaohitaji upasuaji wa ubongo kutoka kaunti jirani huwa wanaletwa hapa kuhudumiwa.” Alisema.