HOSPITALI YA RUFAA TRANS NZOIA YAFUNGULIWA RASMI.

Gavana wa Kaunti ya Trans Nzoia Patrick Khaemba amefungua rasmi  hospitali kuu ya mafunzo na rufaa mjini Kitale, na kuanza kutoa  huduma za afya  na vipimo kwa magonjwa kama vile kisukari, shinikizo la damu na saratani  kwa wenyeji wa Kaunti hiyo.

Akihutubu kwenye hafla ya ufunguzi wa hospitali hiyo Gavana Khaemba amesema Hospitali hiyo itatoa huduma mbalimbali za matibabu  kwa wenyeji wa Kaunti ya Trans Nzoia na kuwapunguzia gharama ya usafiri  kutafuta matibabu  maeneo mengine mbali na kutoa huduma za afya  kwa Kaunti jirani kutokana na vifaa vya hali ya juu vya matibabu vitakavyowekezwa kwenye hospitali hiyo.

Wakati huo huo Khaemba amesema kufunguliwa kwa Hospitali hiyo kumeongeza idadi ya vitanda vya kulazwa wagonjwa kutoka 380 hapo awali hadi vitanda 910.

Kwa upande wake  mwenyekiti wa tume ya ugavi wa rasilimali kwa serikali za Kaunti Jane Kerengai amesifia ujenzi wa Hospitali hiyo akitaja kuwa ni moja wapo ya matunda ya ugatuzi katika Kaunti ya Trans Nzoia.