HOSPITALI YA KAPENGURIA YAPOKEA DAWA ZAIDI KUTOKA KEMSA.

Huduma za afya zinatarajiwa kuimarika katika hospitali na zahanati za kaunti ya Pokot magharibi baada ya serikali ya kaunti hiyo kupokea dawa lori saba kutoka katika shirika la kusambaza dawa na vifaa vya matibabu KEMSA.

Akizungumza baada ya kupokea dawa hizo gavana Simon Kachapin alisema kwamba dawa hizo zitasambazwa katika vituo vyote vya afya katika kaunti hiyo huku akiwataka maafisa watakaohusika katika kusambaza dawa hizo kuzingatia uadilifu katika shughuli hiyo.

“Tumepokea dawa nyingi sana kutoka KEMSA na hivyo natumahi kwamba watu wetu watapata dawa kwa wingi katika hospitali na zahanati zetu bila tatizo. Na wale wanaopewa jukumu la kusambaza dawa hizi wazingatie uadilifu na kuhakikisha zinasambazwa vizuri kwa zahanati zote.” Alisema Kachapin.

Wakati uo huo Kachapin alisema kwamba atafungua rasmi zahanati alizojenga katika awamu yake ya kwanza ya uongozi na ambazo hazijaanza kuhudumu kando na kuajiri wahudumu zaidi wa afya kuwahudumia wakazi wa maeneo mbali mbali ya kaunti hiyo.

“Zahanati ambazo nilijenga na hazijaanza kazi mimi mwenyewe nitazianzisha. Ila naona tayari baadhi zinafanya kazi. Zile chache zilizosalia tuhakikisha kwamba tunafungua na tuwe na maafisa wa kuhudumia watu kule. Nitaajiri wahudumu wa afya wa kutosha kuhakikisha huduma kwa watu wetu.” Alisema.

Kando na hayo Kachapin alitumia fursa hiyo kuwahakikishia wakazi wa Pokot magharibi kwamba serikali yake inaendeleza mikakati ya kuhakikisha yapo maji ya kutosha kupitia uchimbaji mabwawa ili kuendeleza kilimo cha unyunyiziaji maji mashamba katika juhudi za kuhakikisha usalama wa chakula.

“Tumekuwa na wadau mbali mbali katika sekta ya maji na tumezungumzia mipango ya kuchimba mabwawa maeneo mbali mbali ya kaunti hii. Nia yangu ni kuhakikisha kuwa tunaendeleza kilimo cha kunyunyizia maji mashamba kuhakikisha usalama wa chakula kaunti hii.” Alisema Kachapin.