Hospitali ya Kapenguria yapania kuimarisha huduma kwa kubadilisha mfumo wake

Chumba cha wagonjwa katika Hospitali ya rufaa ya Kapenguria, Picha/Maktaba
Na Benson Aswani,
Uongozi wa hospitali ya Kapenguria katika kaunti ya Pokot magharibi umetoa wito kwa wanaofika kutafuta huduma za afya katika hospitali hiyo kuwa na subira wakati huu ambapo hospitali hiyo inaendelea kufanyia mabadiliko mfumo wake wa kutoa huduma.
Akizungumza na kituo hiki daktari mkuu wa hospitali hiyo Dkt. Simon Kapchanga alisema kwamba huenda mchakato wa kubadilisha mfumo huo ukaathiri jinsi ambavyo huduma zinatolewa, ila akatoa hakikisho kwamba hali itarejea kawaida baada ya shughuli hiyo kukamilika.
“Tunabadilisha mfumo wetu na kutokana na mabadiliko hayo kutakuwa na changamoto kidogo katika kutoa huduma kwa kuwa mfumo mpya huja na mambo mapya. Lakini tuna uhakika baada ya muda mfupi changamoto hizo zitatatuliwa na huduma zirejee kawaida,” alisema Kapchanga.
Kulingana na Kapchanga, mfumo huo mpya utasaidia katika kuimarisha na kurahisisha huduma za matibabu katika hospitali hiyo ikilinganishwa na jinsi ambavyo shughuli zilikuwa zikiendeshwa katika mfumo wa sasa.
“Huu mfumo utasaidia pakubwa kuimarisha huduma katika hospitali hii kwani unasaidia kufuatilia jinsi huduma zinafanyika katika kila idara,” alisema
Wakati uo huo, Kapchanga alikanusha madai kwamba hali ya usafi katika hospitali hiyo ni duni kutokana na changamoto ya maji, akisisitiza kwamba hamna wakati ambapo hospitali hiyo imekosa bidhaa hiyo.
“Kumekuwa na dhana kwamba kuna tatizo la maji hali ambayo inachangia katika hali duni ya usafi. Nataka kusema kwamba huo si ukweli kwa sababu tuna mbinu mbali mbali za kupata maji na mbinu hizo zote zinafanya vyema,” aliongeza.