HOSPITALI YA KACHELIBA YAKANUSHA MADAI YA KUTOKUWEPO DAWA ZA KUTOSHA.


Uongozi wa hospitali ya level four ya Kacheliba kaunti hii ya Pokot magharibi umekanusha madai ya kuwepo ukosefu wa dawa katika hospitali hiyo.
Akizungumza afisini mwake, msimamizi mkuu wa hospitali hiyo Solomon Tukei amesema kuwa hospitali hiyo ina dawa za kutosha na za kila aina ya magonjwa baada ya kupokea shehena ya kwanza mwezi mmoja uliopita na huku ya pili ikipokelewa siku ya ijumaa juma lililopita.
Tukei amewataka wakazi wa eneo hilo kupuuza madai yanayoenezwa kuwa hospitali hiyo ina upungufu wa dawa, akisema dawa ambazo huenda zikakosekana kupatikana ni za magonjwa ambayo hutokea kwa nadra sana.
Ni kauli ambayo imesisitizwa na muuguzi mkuu wa hospitali hiyo Luke Kanyang’areng ambaye pia amewahakikishia wakazi wa kacheliba kuwa zipo dawa za madhara yanayosababishwa na kuumwa na nyoka, huku pia akitoa wito kwa serikali ya kaunti kuhakikisha hospitali hiyo inapata ambulansi nyingine kwani iliyopo kwa sasa haitoshelezi mahitaji.
Kauli ya uongozi wa hospitali hiyo inajiri wakati ambapo wakazi wa eneo hilo wamekuwa wakilalamikia ukosefu wa dawa za kutosha katika hospitali hiyo huku serikali ya kaunti hii ya Pokot magharibi ikishutumiwa pakubwa kwa kuitelekeza sekta hiyo ya afya.