HOSPITALI YA KACHELIBA YAKABIDHIWA MTAMBO WA JENERETA KUKABILI TATIZO LA NGUVU ZA UMEME.
Wakazi wa eneo la Kacheliba katika kaunti ya Pokot magharibi wamepata afueni baada ya serikali ya kaunti kupitia idara ya afya kuikabidhi hospitali ya Kacheliba mtambo wa jenereta ambao utatumika katika kuleta mwangaza na huduma zingine katika hospitali hiyo.
Ni hatua ambayo imejiri kufuatia changamoto za kupotea kila mara nguvu za umeme kwenye hospitali hiyo hali ambayo imetajwa kusababisha mahangaiko miongoni mwa wagonjwa ambao wamekuwa wakikosa huduma muhimu kufuatia hali hiyo.
Ni hatua ambayo ilichangamikiwa pakubwa na wakazi wa eneo hilo.
“Napongeza sana serikali ya kaunti chini ya gavana Kachapin kwa kuhakikisha kwamba tunapata suluhu kwa tatizo la nguvu za umeme kupotea kila wakati. Wagonjwa wamekuwa wakihangaika sana kwa kukosa huduma muhimu kutokana na changamoto ya nguvu za umeme.” Walisema.
Wakazi hao walitumia fursa hiyo kuisuta pakubwa kampuni ya kusambaza umeme KPLC kwa kutomakinika katika majukumu yao ya kuhakikisha kwamba swala la kupotea kila mara nguvu za umeme katika hospitali hiyo linashughulikiwa.
“Hawa watu wa KPLC wametutatiza sana hapa Kacheliba. Umeme unapotea kila mara lakini hatuoni wakichukua hatua zozote kushughulikia hali. Tunawaomba kutekeleza kazi yao na kuhakikisha kwamba kuna umeme eneo hili la Kacheliba.” Walisema.
Wakati uo huo wakazi hao waliitaka serikali ya kaunti kushughulikia changamoto zingine ambazo zinawakumba hasa huduma duni za afya, ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana pamoja na barabara mbovu.