HOJA YA KUMBANDUA SPIKA YAWASILISHWA KATIKA BUNGE LA POKOT MAGHARIBI.


Hatima ya spika wa bunge la kaunti hii ya pokot magharibi Catherine Mukenyang sasa imo mikononi mwa wabunge katika bunge hilo baada ya kuwasilishwa hoja ya kumbandua afisini.
Akiwasilisha hoja hiyo mwakilishi wadi ya Endough Evanson Lomaduny amemlaumu Mukenyang kwa kile amedai matumizi mabaya ya afisi, kwenda kinyume na katiba, kutotekeleza majukumu yake ipasavyo na kutozingatia maadili mema katika majukumu yake miongoni mwa madai mengine.
Mukenyang sasa ana siku tano kufika mbele ya kamati ya bunge hilo kujitetea dhidi ya tuhuma ambazo zimewasilishwa dhidi yake.
Mukenyang ambaye ni mmoja wa maspika wa mabunge ya kaunti wa kike wawili pekee waliosalia amekuwa katika mgogoro kwa muda sasa na bunge hilo baada yake kuitisha kikao kilichopingwa na kiongozi wa wengi pamoja na wa wachache katika bunge hilo.