HISIA ZAGHUBIKA KUBANDULIWA AFISINI SPIKA MUKENYANG.
Hatua ya kubanduliwa afisini spika wa bunge la kaunti ya Pokot magharibi Catherine Mukenyang na wabunge katika bunge hilo imeendelea kuibua hisia mseto miongoni mwa wakazi kaunti hii.
Wakiongozwa na James Mariech baadhi ya wakazi wameunga mkono hatua hiyo ya waakilishi wadi wakidai kuwa itaimarisha sasa utendakazi wa bunge hilo ikizingatiwa si mara ya kwanza mukenyang kuondolewa kazini kwani pia maliwahi kufutwa kazi na serikali iliyotangulia kutokana na madai ya utepetevu.
Hata hivyo baadhi ya wakazi wamelaani vikali hatua hiyo wakisema Mukenyang angeruhusiwa kutamatisha muhula wake ikizingatiwa alikuwa amesalia na muda mchache kabla ya kujiuzulu ikizingatiwa alikuwa ametangaza nia ya kugombea kiti cha kisiasa katika uchaguzi mkuu ujao.
Aidha wameitaja hatua hiyo kuwa iliyochochewa kisiasa, wakilaumu uongozi wa kaunti hii kwa kuchochea masaibu yanayomkumba spika huyo wa zamani.