HISIA ZAENDELEA KUIBULIWA KUHUSU KUBUNIWA CHAMA KIPYA POKOT MAGHARIBI.


Siku chache tu baada ya baadhi ya viongozi katika kaunti hii ya Pokot magharibi wakiongozwa na mwakilishi wadi maalum Elijah Kasheusheu kupuuzilia mbali kubuniwa chama kipya katika kaunti hii ya Pokot magharibi, mbunge wa pokot kusini David Pkosing amesema kuwa mikakati inaendelea ya kubuniwa chama hicho.
Pkosing ambaye ni mmoja wa viongozi ambao wako msitari wa mbele katika kuhakikisha chama hichbo kinabuniwa, amesema kuwa wameamua kuchukua hatua hii ili kutoa nafasi kwa jamii ya pokot kuwa na nguvu katika kujadili maswala ambayo yanahusu jamii hii, na sasa kinachoendelea ni kuwaelimisha wakazi kuhusu kubuniwa chama hicho.
Aidha Pkosing amesema kuwa chama hicho ambacho kitaongozwa na gavana wa kaunti hii ya pokot magharibi John Lonyangapuo ambaye pia atahudumu kama msemaji wa chama huku yeye akiwa naibu kinara, hakitajumuisha jamii ya pokot pekee bali kitajumuisha pia jamii za marakwet, maasai pamoja na Somali.
Amesema kuwa kwa muda sasa jamii ya pokot imekuwa ikiunga mkono vyama vingine na kuvisaidia kupita katika chaguzi ambazo zimekuwa zikiandaliwa nchini ila hakijanufaika kwa vyovyote kutokana na uungwaji mkono wa vyama hivyo, na sasa ni wakati wa jamii kujisimamia na kuwa na usemi katika siasa za taifa hili kupitia kubuniwa chama.