Hatutaruhusu ukeketaji kuharibu kizazi kijacho, Kiprop

Vifaa Vinavyotumika Kwa Ukeketaji,Picha/Maktaba
Na Emmanuel Oyasi,
Miito imeendelea kutolewa kwa wazazi katika kaunti ya Pokot magharibi kuwalea vyema wanao na kuhakikisha kwamba wanapata haki zao za kimsingi badala ya kuwalazimishia tamaduni zilizopitwa na wakati za ukeketaji na ndoa za mapema.
Naibu kamishina eneo la Kacheliba Kenneth Kiprop alisema kwamba ni jukumu la wazazi kuwaelekeza vyema wanao na kuhakikisha kwamba wanapata elimu ambayo itawafaa zaidi katika siku zao za usoni.
Kiprop alisema wengi wa watoto wa kike ambao wanalazimika kupitia tamaduni hizi wamekuwa wakikumbana na changamoto tele ikiwemo matatizo ya uzazi pamoja na magonjwa mbali mbali yanayoambatana na ukeketaji kama vile nasuri.
“Kitu ambacho ninawashauri wazazi ni kuhakikisha kwamba wanazingatia malezi bora kwa wanao na kuwaelekeza panapofaa. Watoto wetu waelimishwe ili wawe watu wenye umuhimu mkubwa katika jamii siku za usoni,” alisema Kiprop.
Hata hivyo Kiprop alisema zipo juhudi ambazo zinaendelezwa na serikali kupitia wadau mbali mbali ikiwemo machifu, wazee wa mitaa na mashirika mbali mbali ya kijamii kwa kuendeleza uhamasisho dhidi ya tamaduni hizi zilizopitwa na wakati.
“Kama serikali tumejikakamua kupitia kwa machifu, wazee wa mitaa na wadau mbali mbali ikiwemo mashirika ya kijamii kwa kuendeleza uhamasisho kwa wananchi kuhusu athari za tamaduni hizi potovu,” aliongeza.