HATUA YA RAIS RUTO KUKUTANA NA JAJI MKUU YAENDELEA KUVUTIA HISIA MSETO.

Rais William Ruto na CJ Koome Martha.

Na Emmanuel Oyasi.

Hisia mseto zimeendelea kuibuliwa kufuatia hatua ya rais William Ruto kukutana na jaji mkuu Martha Koome miongoni mwa maafisa wengine kutoka idara ya mahakama na serikali katika ikulu, kuangazia mivutano ambayo imekuwepo baina ya rais na idara hiyo ya mahakama.

Baadhi ya wakazi wa kaunti ya Pokot magharibi wameunga mkono hatua hiyo ya rais kukutana na jaji mkuu wakisema itasaidia kuhakikisha kwamba idara za serikali zinafanya kazi kwa pamoja kuimarisha huduma kwa mwananchi.

“Hatua ya rais kukutana na jaji mkuu ni muhimu sana katika kuhakikisha kwamba idara zote za serikali zinafanya kazi kwa umoja  na kuhakikisha huduma bora kwa wananchi.” Walisema.

Hata hivyo baadhi ya wakazi walikosoa hatua hiyo wakisema kwamba huenda ikapelekea uhuru wa mahakama kuhujumiwa na pia kuathiri kesi zinazohusu serikali ambazo zipo mahakamani.

Walimtaka jaji mkuu Martha Koome kutoshawishiwa na serikali kwenda kinyume cha katiba na badala yake kusimama imara na kuhakikisha kwamba mahakama inatekeleza majukumu yake kulingana na sheria.

“Hatua hii si nzuri wakati huu ikizingatiwa kwamba sasa kuna kesi dhidi ya serikali ambazo zinasubiri kutolewa uamuzi. Huenda kikao hiki kikaathiri maamuzi hayo ya mahakama. Tunachomhimiza jaji Koome ni kushikilia msimamo wake na kutotikiswa na hatua za serikali.” Walisema.