HATIMA YA KESI KUHUSU MATOKEO YA URAIS KUBAINIKA LEO.
Macho yote sasa yameelekezwa kwa jopo la majaji saba wa Mahakama ya juu wanapotarajiwa kutoa uamuzi wao kuhusiana na kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa agosti 9 mwaka huu.
Ni uamuzi unaotarajiwa baada ya jopo hilo kukamilisha vikao vya kusikiliza kesi hiyo ijumaa juma jana na kutumia wikendi yote kuandika uamuzi wao.
Katika uamuzi wa kwanza, majaji saba wa mahakama hiyo wanaweza kudumisha ushindi wa rais mteule dkt. William Ruto kwa kusema kwamba uchaguzi wa agosti 9 uliandaliwa kwa njia huru wazi na kuambatana na katiba.
Hata hivyo kwenye uamuzi wa pili majaji hao wanaweza kufutilia mbali uchaguzi wa urais na kuagiza mwingine kuandaliwa ndani ya siku 60 kuambatana na katiba, uamuzi utakaowapa ushindi walalamishi kwenye kesi iliyowasilishwa mahakamani.
Kulingana na baadhi ya wachanganuzi wa maswala ya kisheria, uamuzi utakaotolewa utajikita katika ushahidi uliowasilishwa mahakamani na pia iwapo uchaguzi uliandaliwa kulingana na sheria za nchi.
Hayo yakijiri rais mteule dkt. Ruto alisema kuwa atakubali uamuzi utakaotolewa na mahakama ambapo pia amewataka waliowasilisha kesi ya kupinga ushindi wake kuridhia uamuzi wa majaji.
Kwa upande wake kinara wa muungano wa azimio one kenya raila odinga akiongea baada ya kukutana na viongozi kutoka kaunti ya meru wanaomuunga mkono alielezea imani kwamba majaji wa mahakama hiyo watatoa uamuzi wa haki.
Uamuzi huo unatarajiwa kujitika katika maswala manane makuu ikiwa ni pamoja na teknolojia ya uchaguzi iliyotumiwa na tume ya IEBC kusimamia uchaguzi mkuu, iwapo mchakato wa kuweka fomu ya 34a katika wavuti wa IEBC ilidukuliwa inavyodaiwa, na iwapo tume hiyo ilithibitisha matokeo kabla ya kutangazwa inavyohitajika kisheria.
Swala jingine ni iwapo kuahirishwa kwa uchaguzi kwenye maeneo manane nchini kulitatiza idadi ya watu waliojitokeza kupiga kura, iwapo Ruto aliafikia ushindi wa asilimia 50 na kura moja na iwapo sheria ilizingatiwa kwa jumla wakati wa uchaguzi mkuu.
Majaji hao pia wanatazamiwa kutoa uamuzi kuhusu iwapo idadi ya wapiga kura walioshiriki katika kipute cha ikulu ilizidi ya wale walioshiriki chaguzi za nyadhifa zingine na iwapo tofauti za makamishina wa IEBC zilitatiza shughuli ya kuthibitisha matokeo.