HAMASISHO YATOLEWA KWA UMMA KUHUSU UMUHIMU WA KUDAI FIDIA BAADA YA AJALI

Umma umetakiwa kufuata taratibu zinazostahili panapotokea ajali ili kuhakikisha haki inatendeka kwa mwathiriwa.
Akitoa hamasisho kwa wakazi wa kaunti hii ya Pokot magharibi kuhusu umuhimu wa kufuata fidia, wakili Philip Magal amesema kuwa magari au pikipiki zina bima ambayo inastahili kugharamia madhara yoyote ambayo yamesababishwa na gari au pikipiki husika.
Magal ametaka umma kutojihusisha katika makubaliano ambayo huenda yakapelekea mwathiriwa wa ajali kutopata haki na badala yake kufuata taratibu ambazo zinastahili kulingana na sheria zilizopo.
Wakati uo huo Magal ametoa wito kwa maafisa wa polisi kufuata pia taratibu zinazostahili katika kushughulikia ajali za barabarani na kutotumika kuhujumu waathiriwa na badala yake kuwasaidia ili kuhakikisha wanafidiwa panapostahili.