HALI YA USALAMA YATIWA KWENYE MIZANI BONDE LA KERIO KUELEKEA UCHAGUZI MKUU.
Uchaguzi mkuu wa agosti 9 ukitarajiwa kuandaliwa hapo kesho, waathiriwa wa uvamizi katika eneo bunge la baringo kaskazini na kusini sasa wanaitaka serikali kuimarisha usalama katika maeneo hayo ili kuwawezesha kushiriki katika zoezi hilo.
Katika eneo bunge la baringo kaskazini waathiriwa hao waliojiandikisha kupiga kura katika vituo vya kagir, chemoe na yatya wanasema kuwa walilazimika kutoroka makwao kutokana na uvamizi wa mara kwa mara kutoka kwa wezi wa mifugo.
Joseph kibet mmoja wa wakazi hao anasema kuwa huwenda wengi wao wakakosa kushiriki katika shughuli ya upigaji wa kura iwapo hawatahakikishiwa usalama wao.
“kwa area yetu ya Kakir, Yatya, Ng’aratuko, hayo ameneo yote ambayo hayana usalama, nataka serikali wasaidie, waongeze security ya kutosha wakati wa kupiga kura ili tutekeleze haki yetu ya kupiga kura.” Amesema Kibet.
Waathiriwa hao ambao kwa sasa wanaishi kwenye makambi katika maeneo ya rondinin na chesegem aidha wanairai serikali kuwasafirisha hadi kwenye vituo vyao vya kupigia kura ili kutekeleza wajibu wao wa kikatiba wa kuwachagua viongozi wanaowataka.
“Tunaomba usalama kwanza. Watutafutie namna ya kufika sehemu kama Kakir, Yatya, Ng’aratuko, Kosile kwa sababu sasa tunaona usalama si sawa.” Wamesema wakazi.
Katika eneo bunge la baringo kusini, huwenda baadhi ya wakazi waliojiandikisha kupigia kura zao katika vituo vya sinoni, chebinyiny, arabal, na lamaiywe wakakosa kupiga kura baada yao kutoroka makwao kufuatia uvamizi wa mara kwa mara.