HALI YA USALAMA MIPAKANI YAZIDI KUWAKEKETA MAINI VIONGOZI POKOT MAGHARIBI.

Aliyekuwa mwakilishi wadi ya Masol eneo bunge la Sigor katika kaunti ya Pokot magharibi Ariong’o Loporna amezitaka asasi za usalama kuimarisha usalama maeneo ya mipakani pa kaunti hii ya Pokot magharibi na kaunti jirani ya Elgeyo marakwet.

Loporna alisema kwamba mifugo wa wakazi wengi wa eneo hilo wameibwa kufuatia visa vya uvamizi unaotekelezwa na wezi wa mifugo kutoka kaunti jirani, akisema ni wakati serikali inapasa kuchukua hatua za dharura kukomesha uhalifu huu.

“Watu wetu wamepoteza mifugo wao wengi mikononi mwa wezi kutoka kaunti jirani. Hata wengine wameuliwa katika visa hivyo. Tunataka idara ya usalama kumakinika na kutia kikomo kwa uhuni huu ambao umekosesha amani ya wakazi wengi. Wapo wakazi wengi ambao wamepoteza hata maisha yao kufuatia uhalifu huu.” Alisema Ariong’o.

Ariong’o alisema kwamba licha ya mikutano ya amani ambayo inaandaliwa mara kwa mara na wadau kutoka pande zoteza pokot magharibi na Elgeyo marakwet, hamna hatua zozote ambazo zimepigwa kutia kikomo visa hivi kwani vimeendelea kushuhudiwa.

“Uvamizi umeendelea tu kuripotiwa maeneo haya licha ya viongozi kutoka kaunti ya Pokot magharibi na kaunti ya Elgeyo marakwet kuandaa mikutano ya kumaliza visa hivi. Tunaomba wakazi wa maeneo haya kusitisha uovu huu na kuishi kwa amani.” Alisema.