HALI YA KIANGAZI YAENDELEA KUWATIA HOFU WAKULIMA WA MIFUGO POKOT KUSINI.


Hali ya kiangazi ikizidi kushuhudiwa katika maeneo mbalimbali nchini, Wakulima wa mifugo hasa ngombe kutoka eneo la Sepuser wadi ya Chepareria eneo bunge la pokot kusini kaunti ya Pokot Magharibi wanahitaji msaada wa dharura kutoka Idara ya kilimo kaunti hiyo ili kunusuru mifugo wao kutokana na makali ya njaa.
Wakiongozwa na Geofry Toroitich wakulima hao walisema iwapo hali itaendelea jinsi ilivyo watapoteza mifugo wao jambo ambalo limewafanya hata kukosa maziwa ambayo ni bidhaa muhimu kwao kama kitega uchumi.
“Sisi wakazi wa Sepuser tunategemea sana ufugaji wa ng’ome ila kwa sasa hali si nzuri. Kiangazi kimekithiri mno hadi imekuwa vigumu sana kupata chakula cha mifugo. Iwapo hali hii itaendelea tutapoteza mifugo wetu.” Alisema Toroitich.
Aidha Toroitich alisema, “Mito huku imekauka na tunalazimika kwenda mwendo mrefu kutafuta maji kwa ajili ya mifugo wetu. Maziwa yamepungua kabisa kwa sababu ya njaa na sasa hatuna maziwa kuuza hali tumekuwa tukiyategemea zaidi kama kitega uchumi kwetu.” Alisema.
Wakati uo huo wakulima hao wameirai serikali kuanza kutoa mafunzo kwa wakulima kufahamu mbinu za kisasa za kuendeleza kilimo hicho pamoja na kuwapa mbegu za nyasi kando na kuwachimbia visima vya vya maji.
“Ingekuwa vyema zaidi iwapo serikali ya kaunti hasa maafisa wa kilimo wangetupa mafunzo kuhusu mbinu za kisasa za ufugaji. Pia tunaomba kupewa mbegu za nyasi ili tupande msimu wa mvua utakapoanza ili tuepuke hali kama hii siku za usoni.” Walisema wakulima.

[wp_radio_player]