HAFLA ZA MICHANGO KACHELIBA ZAPIGWA MARUFUKU HADI ITAKAPOKALIMIKA MITIHANI YA KITAIFA.
Idara ya usalama eneo la Kacheliba kaunti ya Pokot magharibi imepiga marufuku mikutano ya michango ya silk eneo hilo hadi itakapokamilika mitihani ya kitaifa hasa wa darasa la nane ambao unaanza wiki ijayo ili kuwapa watahiniwa nafasi ya kufanya mitihani hiyo bila ya usumbufu wowote.
Akizungumza katika hafla moja eneo hilo, naibu kamishina wa Kacheliba Kenneth Kiprop alisema kwamba hafla hizo za michango huambatana na kelele ambazo huenda zikasababisha mazingira ambayo si salama wakati watahiniwa wakiendelea na mitihani yao ya kitaifa.
Aidha Kiprop alionya dhidi ya kuwahusisha watoto katika hafla hizo za michango ambazo alisema kwamba huandaliwa hadi nyakati za usiku na kupelekea mazingira ambayo ni hatari kwa maisha yao, akitoa wito kwa viongozi wa kisiasa kushirikiana na idara za usalama katika kuhakikisha agizo hilo linazingatiwa.
“Kuanzia sasa hadi mitihani ya kitaifa kwa darasa la nane KCPE itakapokamilika tumepiga marufuku hafla zozote za michango hasa Silk. Tunawaomba viongozi wa kisiasa ambao ndio hualikwa sana katika michango hiyo kushirikiana nasi kuhakikisha kwamba watoto wetu wanapata wakati mzuri wa kufanya mitihani bila ya usumbufu wa kelele ambao huambatana na hafla hizo za michango.” Alisema Kiprop.
Wakati uo huo Kiprop aliwataka OCPD na OCS wa eneo hilo kutotoa leseni kiholela za kuandaliwa hafla hizo, na badala yake kushirikiana na machifu ili kubaini ni hafla za aina gani ambazo zinaandaliwa, ili kuzuia matukio ambayo yanachangia kupotoka maadili miongoni mwa vijana.
“OCPD na OCS wa eneo hili wasitoe tu leseni kiholela kwa watu ambao wanaandaa hafla mbali mbali bali wanapasa kushirikiana na machifu ili kubaini ni hafla gani ambazo zinaandaliwa. Tusije tukapeana leseni za kuandaliwa hafla mbazo huenda zikawa hatari kwa watoto wetu.” Alisema.