GHARAMA YA MAISHA YAENDELEA KUKEKETA MAINI YA WAKENYA MAENEO MBALI MBALI.

Baadhi ya wakazi wa kaunti hii ya Pokot magharibi wamelalamikia uongozi wa rais William Ruto wanaosema kwamba umepelekea kupanda maradufu gharama ya maisha nchini tangu alipoingia uongozini.

Wakizungumza baada ya kushiriki maandamano yaliyoitishwa na kinara wa chama cha muungano wa azimio la umoja one Kenya Raila Odinga, wakazi hao walisema kwamba rais Ruto aliwahadaa wakenya kwamba angepunguza gharama ya maisha punde atakapoingia madarakani ila sasa hali ni tofauti wakihisi kuhadaiwa.

“Rais Ruto alisema kwamba atapunguza gharama ya maisha punde akiingia mamlakani, ila sasa tunashangaa ni kwa nini hadi sasa gharama ya maisha imeendelea kupanda. Ametuhadaa sana sisi kama wakenya tuliomuunga mkono.” Walisema.

Aidha wakazi hao waliapa kushiriki maandamano hayo wakati wowote yakiitishwa na kinara wa azimio Raila Odinga wakimtaka rais Ruto kusikiliza kilio cha wakenya na kupunguza gharama ya maisha kwani ni wao ndio waliomwezesha kuingia madarakani.

“Tutaandamana kila wakati maandamano yataitishwa kwa sababu sasa tumechoka na ahadi bure ambazo zinatolewa na rais. Ni wananchi ndio walimchagua rais Ruto na ni wananchi ndio tulio na mamlaka ya kumwondoa afisini. Kwa hivyo asikilize wananchi.” Walisema.

Kauli za wakazi hawa zilisisitizwa na mwakilishi wadi maalum Bruno Lomeno ambaye aidha aliwasuta pakubwa maafisa wa polisi kwa kile alisema kutumia nguvu kupita kiasi kuwakabili wananchi wanaoshiriki maandamano akisema ni haki yao kikatiba kuandaa maandamano kushinikiza kupunguzwa gharama ya maisha.

“Katiba inawapa wakenya uhuru wa kuandamamana. Kwa hivyo wakenya wanaoandamana wamelindwa kikatiba. Haya mazoea ya polisi kutumia nguvu kupita kiasi kuwakabili wananchi ambao wanatekeleza jukumu lao kikatiba hayafai hata kidogo.” Alisema Bruno.