GAVANA WA POKOT MAGHARIBI APONGEZWA KWA KUORODHESHWA WA TATU NCHINI KATIKA UTOAJI HUDUMA KWA WANANCHI.
Wadau mbali mbali kaunti ya Pokot magharibi wameendelea kupongeza hatua ya kuorodheshwa gavana Simon Kachapin katika nafasi ya tatu katika ripoti iliyotolewa na kampuni ya utafiti ya Infortrack kuhusiana na utendakazi wa magavana nchini.
Afisa mkuu katika idara ya mipango maalum na majanga kaunti hiyo Lilian Korinyang alisema kwamba gavana Kachapin alistahili nafasi hiyo kutokana na yale ambayo ametekeleza ndani ya kipindi cha mwaka mmoja tangu alipoingia afisini.
Korinyang alisema uhusiano mwema ambao gavana Kachapin amejenga kati ya afisi yake na maafisa katika serikali yake, umepelekea ushirikiano katika kila sekta, hali ambayo imechangia pakubwa huduma bora ambazo zinatolewa na serikali yake kwa wananchi.
Aidha alielezea matumaini kwamba mikakati ambayo gavana Kachapin ameweka kuimarisha huduma kwa wananchi itapelekea kaunti hiyo kuimarika zaidi na hata kuorodheshwa bora zaidi katika utoaji huduma kwa wananchi.
“Gavana wetu ameorodheshwa katika nafasi ya tatu katika utendakazi wa magavana nchini. Kazi yake imeonekana kwa huu muda mfupi ambao amekuwa afisini. Uhusiano mzuri ambao amekuwa nao na maafiosa katika serikali yake umechangia pakubwa kuimarishwa huduma kwa wananchi kaunti hii.” Alisema Korinyang.
Wakati uo huo Korinyang alielezea mipango ya serikali kupitia idara ya mipango maalum kuhakikisha kwamba wakazi maeneo mbali mbali kaunti hiyo wanapata msaada wa chakula baada ya mimea kukosa kufanya vyema maeneo hayo kufuatia hali ya ukame ambayo imekithiri.
“Kama idara ya majanga tunafahamu kwamba tuna changamoto kubwa sana kuhusiana na swala la chakula kutokana na hali ya ukame ambao umeshuhudiwa maeneo mbali mbali ya kaunti hii. Tuna mipango ya kuhakikisha kwamba wakazi wa maeneo hayo wanapata chakula.” Alisema.